Tuesday, February 28, 2023

Hiki ndicho kinachotupoteza

Katika zama tulizomo kuna vitu ambavyo tumevipa nguvu na vimefanya tukose usingizi. Ila kuna kitu bado tunakipuuzia. 

Huenda umekuwa unajiuliza kwanini ajali nyingi zinazidi kutokea, na kwa nini haziishi licha ya uwepo wa askari usalama barabarani sehemu nyingi? Na sheria kali. 

Jibu ni moja tunakosa umakini. 

Kwanini siku hizi majibu ya mitihani kwa watoto wetu hayaridhishi kwa kiwango cha juu? Jibu ni moja tu hakuna umakini. 

Kwa nini biashara nyingi zinakosa kuwa na mauzo mazuri, licha ya kuwepo mwa mzigo wa maana. Jibu ni moja umakini. 

Umakini ni suala ambalo wengi wetu tumelipiga kisogo. Tunaweka jitihada kujifunza tena kwa kulipia, wakati mwingine kununua baadhi ya vitu ili tusonge mbele kwa kukosa umakini tunashindwa kuvifanikisha. 

Siku hizi suala la kukuta mtu anaongea na simu wakati akiwazaa kitu kingine ni la kawaida. Yaani anongea na simu ya muhimu huku yeye akiwa na kitu kingine kisicho muhimu anachokikazania. Ndio maana mwisho wa mazungumzo ukimuuliza mlichozungumza anashangaa. Ndio uhalisia tulionao. 

Tumepoteza umakini kwa kiwango cha juu. Tunakoelekea sio kuzuri. Faini zimewekwa za kutosha mfano dereva hupaswi kuendesha mwendo fulani huwapo sehemu fulani. Kwani wanasikia basi. Tunaambiwa kuovertake gari ni hatari. Lakini ajali ngapi hutokea? Ni kukosa umakini. 

Hata kwenye familia janga lipo kubwa. Mtu anapika chakula lakini akili yake ipo kwenye TV ili aangalie tamthiliya fulani. Matokeo yake chakula kinaungua. Mume akija vurugu zinaanza. 

Walio kwenye mahusiano ya kawaida pia. Mtu yupo na mwezi wake lakini mawazo yake yapo mahali pengine. Unaweza kushangaa lakini ndio ukweli. Au unaweza kuwa unaongea na mtu anakutazama lakini ukimuuliza kitu anashtuka au anashangaa sana. Ni kwa sababu hajaweka umakini kwako. 

Wengi tunaruhusu vivuli vyetu kuwa mbele za watu. Upo na mtu karibu lakini mawazo na kila kitu havipo hapo. Hiyo hali sio sawa. Wakati ni sasa. Weka umakini kwa kitu unachofanya ili ukifanye kwa uzuri zaidi. 

Weka moyo wako na akili zako zote kwa kitu unachofanya. Hakika utakifanikisha. 

Je, ni nini kinakufanya ukose umakini? 

Bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
#31mwangaza2023

No comments:

Post a Comment