Sunday, February 26, 2023

Jipongeze mwenyewe

Wakati nasoma sekondari alikuwepo mwalimu mmoja aliyekuwa anapenda kutumia msemo wa "ikiwa watu hawakusifii au kukupongeza kwa kizuri unachofanya unapaswa kujipongeza mwenyewe".

Ni kweli alikuwa anafundisha vizuri katika masomo ya sayansi hasa kemia na fizikia. Wanafunzi wengi waliokuwa wanafaulu  walitoka kwenye masomo yake. 

Wakati anatufundisha alikuwa anapendelea kuutumia msemo tajwa hapo juu. Akimaanisha licha ya kufanya vema shuleni kwa kufundisha kwa moyo wote lakini hakuwa anapata pongezi sahihi. Akawa anatwambia badala ya kukatishwa tamaa na hilo au kusubiri pongezi. Wewe jipongeze mwenyewe. Hii itakupa hamasa kubwa kiutendaji. Alikuwa anajipongeza mwenyewe. 

Ni ukweli usiopingika kuwa zama tulizomo zimekosa subira. Vitu vingi vinawekwa wazi. Hakuna siri tena. Wengi wetu tunaweka picha kwenye mitandao tukisubiri comments na likes kulingana na mahudhui tuliyoweka. Zinapokosa tunaumia sana. Hasa tunapoona wenzetu wanazipata kwa kiwango kikubwa tunaumia zaidi. 

Pengine huchangia kukata tamaa katika baadhi ya kazi zetu. Huku baadhi tukiamini hawatuthamini au kujali kazi zetu. 

Katika hali kama hizi tunaumia sana. Ila ndio ukweli kuwa; dunia imekosa subira. Haipo tayari kukupa pongezi inahitaji ukae au urudi hatua chache nyuma ya ulipo. 

Turudi kwenye msemo wa mwalimu wangu. Aliamua kujipongeza mwenyewe. Hii inaitwa "self recognition" unajipongeza mwenyewe. Lengo kuu ni usichoke wala kukata tamaa au kuacha unachofanya. 

Chukulia mti kama mwembe au mpera. Haujawahi kupongezwa kwa kazi yake badala yake unapigwa mawe na kukatwa. Lakini bado haujawahi kuacha kutoa matunda kila msimu unapofika. 

Hata wewe unahitaji kuweka nguvu katika kazi zako. Waseme wasiseme endelea kuchapa kazi. Jisifu na jipongeze uwezavyo. Itakusaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza hamasa katika utendaji wako. 

Nyakati za furaha, furahia. Nyakati ngumu au uangukapo piga moyo konde endelea na kazi. Utajisogezea baraka na nguvu kubwa. 

Je, wewe unasubiri kupongezwa? 
Bonga nasi hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
#29mwangaza2023

No comments:

Post a Comment