Msemo wa mvumilivu hula mbivu unayo maana kubwa katika maisha ya mwanamafanikio yeyote. Ikiwa huna uvumilivu mambo mengi hutakubali yakupite. Lakini huo ndio ukweli.
Kuna wakati utaweka juhudi kubwa katika kitu fulani lakini huoni matokeo. Sio kwamba unakosea au haupo sawa. Bali muda haujafika. Hakuna aliyefanikiwa katika jaribio la kwanza. Wote walifanya majaribio mengi zaidi yaliyopelekea baadaye kufanikiwa.
Mafanikio yao hayakutokana na juhudi tu bali na uvumilivu mkubwa. Chukulia mtoto mdogo anapozaliwa. Inachukua muda mrefu kuona ameanza kutembea kuongea na kukimbia. Lakini kila mara kuna kitu anakuwa anafanya.
Kadiri muda unavyozidi kwenda ndivyo anavyokuwa anafanikiwa eneo moja. Hawezi kuanza kukimbia moja kwa moja anaanza na kutambaa baadaye kusimama. Kisha kukimbia. Sio zoezi la siku moja wengine inachukua miaka miwili. Katika nyakati hizo mtoto hachoki kuonyesha jitihada kubwa na uvumilivu pale aangukapo. Ni katika kuvumilia ndipo juhudi zetu huzaa matunda.
Kuna wakati unafanya kitu ukiwa na matarajio makubwa lakini hupati matokeo unayoyataka. Ila kwa kuwa una uvumilivu ndani yako unazidi kufanya.
Muda unapofika. Kila kitu kinakuwa sawa. Ndiyo maana ya mvumilivu hula mbivu. Changamoto unazopata au ukinzani unaokutana nao unakujenga zaidi kuwa imara.
Mchanganyiko wa nyakati ngumu huwa haudumu zaidi. Unachohitaji ni kuwa na uvumilivu huku ukiendelea kuonyesha jitihada zako.
Jifunze kuona uwezekano katika nyakati ngumu. Hiyo itakusaidia kuongeza jitihada maradufu. Hakuna kinachoshindikana kwenye uvumilivu na jitihada. Mara zote kuwa mtu wa kufanya. Wewe fanya, hata kama ni wakati mgumu jaribu kufanya. Mambo yatajipa.
Je, ni wakati upi mgumu hutousahahu?
Bonga nasi hapa hapa 0767702659
Imeandaliwa na Lackius Robert
#30mwangaza2023
No comments:
Post a Comment