Tuesday, February 07, 2023

Ni siku nzuri au mbaya kwako?

 Ni swali unalopaswa kujiuliza kila mara uamkapo asubuhi. Maana namna unavyoanza siku yako ni kiashiria tosha kuwa itakuwa nzuri au mbaya. Unaweza kuanza na maombi, tahajudi au mazoezi, kusoma kitabu au kusikiliza redio au mafundisho mazuri yenye hamasa chanya. Kutenga muda asubuhi kujifunza kitu ni muhimu sana, maana itakupa nguvu na kuiangaza siku yako. Japo baadhi yetu hatufanyi hivyo. 

Mwingine ukimwambia kuhusu maombi ya asubuhi, kumshukuru Mungu kwa kumpa nafasi kuona siku nyingine, anaona kama unampotezea muda. Lakini ni muhimu sana kwa mtu mwenye maono makubwa. Muda wa asubuhi ni mzuri sana kupangilia ratiba zako. Hasa hasa baada ya kuwa umepata hamasa kupitia vitu mbalimbali. Binafsi mawazo mengi mazuri huwa ninayapata asubuhi. Hii ni kwa sababu akili yako inakuwa mpya ina nguvu haijavurugwa na kitu chochote, ukiachana na ndoto za usiku. 

Najua umewahi kusikia msemo huu; “umenikuta na akili zangu za asubuhi”. Maana yake umenikuta nipo timamu, sijapigwa na jua, kuvurugwa na usafiri, baba mwenye nyumba au bosi wangu kazini. Akili inakuwa na uwezo mkubwa wa kufikiria. 

Watu wengi waliofanikiwa huwa wanatumia sana muda wao wa asubuhi kupangilia ratiba za siku zao. Katika hili sio lazima utumie muda mwingi sana. Oh! Et masaa manne au matatu. Unaweza kutenga hata dakika 30 au zaidi pengine saa moja kulingana na unavyotaka wewe. Labda kuanzia saa kumi hadi saa kumi na moja asubuhi, au saa kumi na moja asubuhi hadi saa kumi na mbili asubuhi. Wewe tu kulingana na uchaguzi wako. 

Safari ya maili elfu moja huwa inaanza hatua moja. Mafanikio ya wiki, mwezi au mwaka, vyote hujengwa kuanzia siku moja. Ambayo ndio kama hii uliyoamka asubuhi ya leo. 

Yule unayemuona amefikisha miaka mia moja alianza na siku moja. Aliye juu ya mlima hajaibuka tu kupanda mlima, bali alijipanga na kufanya mazoezi aliyokuwa anafanya kwa siku moja. Mchezaji maarufu alianza na mazoezi ya siku moja. Mwandishi maarufu kadharika na wengine. 

Leo ni leo amua ufanye kitu. Hakika lilo jambo utalibadili. Ikiwa kuna changamoto tuwasiliane 0767702659. 

Mimi nimeanza na hii ☝️ wewe je? 

Bonga nasi hapa hapa...

Imeandaliwa na Lackius Robert 

#12mwangaza2023.

No comments:

Post a Comment