Thursday, February 23, 2023

Huku ndipo nguvu zako uanzia

Umewahi kumuona Paka katika sehemu zenye taabu. Ikiwa na maana kwenye jua kali, moto mkali au sehemu hatarishi. Jibu ni hapana. Unataka kujua kwa nini? Twende pamoja.

Tupo katika dunia yenye changamoto nyingi zaidi. Kadri muda unavyozidi kwenda mbele ndivyo zinavyozidi kuongezeka. Kuongezeka kwa changamoto hizi kumewafanya baadhi yetu kukosa utulivu.

Hii imewafanya kila mara wapatapo changamoto kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii kupost n.k. Nia yao kuu ilikiwa ni kupata msaada juu ya magumu yanayowakabili. Matokeo yake imekuwa tofauti na kufanya mfadhaiko kwao kuzidi kuwa mkubwa.

Wanachoshindwa kujua ni kuwa mitandao ya kijamii haiwezi kutatua kila tatizo. Kwa sababu kule unakutana na watu wengine wenye matatizo. Hivyo, tatizo linazidi kuwa sugu. Na kinachoongeza uzito ni kule kusemwa au kusimangwa ambako mtu hukutana nako kwenye mitandao.

Siku ya leo nimekuja na njia mpya kukusaidia kutatua changamoto hiyo. Ukumbuke hapo juu nimeanza kukuuliza swali kuhusu Paka. Namna anavyopenda starehe na kukataa maisha ya shida. Utamkuta amekaa kwenye kochi ametulia. Amekaa kivulini uvunguni mwa gari. Amekaa sehemu ya upepo safi na tulivu. Lengo kuu ni kuponya majeraha anayokutana nayo katika harakati zake za utafutaji wa chakula.

Kwetu binadamu sehemu inayoenda kuwa baraka kwetu ni sehemu yenye utulivu kwa maana ya faragha. Huko ndiko nguvu zinakotoka. Maana unapata nafasi ya kutafakari kwa kina juu ya hali mbalimbali unazopitia katika maisha yako.

Kuna wakati tunaona kama tuna changamoto lakini unapopata muda wa kutafakari utagundua vitu vingi. Uwezekano wa vitu unaanzia kwenye fikra. Akili yako itakuwa na uwezo mkubwa wa kuwaza vitu na kutafuta suluhu. Una changamoto ya mauzo, ndoa, mahusiano  au kazini. Tafuta eneo tulivu utulie kisha ujitakafari zaidi. Mara zote ikumbuke hii "tenga muda wa kufikiri kwa sababu ndipo kuna chanzo kikubwa cha nguvu zako"

Je, uko tayari kutafuta nguvu hizo? Bonga nasi hapa hapa 0767702659

Lackius Robert

#27mwangaza2023

No comments:

Post a Comment