Ni kawaida ya kila anayetembea kuanguka. Au kila anayeweza kusimama. Iwe katika nyakati nzuri au mbaya. Kuanguka kupo tu.
Shida inakuja unaanguka katika mazingira yapi. Je, unaweza kunyanyuka au huwezi? Na ni nani wa kukusaidia?
Huenda hujaelewa point yangu. Ni kweli, umedhamiria kuacha tabia fulani kitu fulani. Kilichokuwa kinakurudisha nyuma. Hasa pale unapokuwa unakifanya.
Inaweza kuwa kulewa, kutembea usiku, kuiba, kuwasema vibaya watu, matumizi ya pesa hovyo. Na mengine mengi.
Umejaribu kila mbinu imeshindikana. Badala ya kusimama umejikuta unaanguka tena. Leo ninao ujumbe mzuri kwa ajili yako.
Inuka, unayo nafasi. Ruhusu mwili wako kuona uwezekano juu ya tabia unayotamani kuiacha. Maana mwili wako, umekuwa unachangia kukupa sababu kwa kiasi kikubwa. Kila unapotaka kujitoa umekuwa unakupa mapingamizi. Unahisi kuchoka na hatua za mabadiliko. Unaona kama haiwezekani kabisa.
Ukweli ni kuwa hii hatua unayotaka kuipiga haitakuwa ya siku moja. Inahitaji ufanye maamuzi magumu. Haya yatapelekea wewe kuingia kwenye mchakato sahihi. Kukaa kwako kwenye mchakato kutakuja na majibu tofauti tofauti.
Mchukulie mtoto mdogo, anapokuwa katika hatua za ukuaji. Kila anapotaka kutambaa au kusimama mwili unagoma. Kinachomsaidia kutoka hapo ni kwamba, anaulazimisha kufanya kile anachotaka kufanya. Inachukua muda lakini baadaye anazoea.
Wakati ndio huu ile tabia inayokuangusha na kukurudisha nyuma kuiwekea mpango wa kuiacha. Inuka, unayo nafasi. Na ni rahisi sana kuifanikisha.
Kuanguka ni jambo la kawaida. Kubakia chini ndio mwiko kabisa wa safari yako. Anguka, inuka, simama na usonge mbele. Ipo nafasi kwa ajili yako.
Imeandaliwa na Lackius Robert 0767702659
#25mwangaza2023
No comments:
Post a Comment