Wednesday, February 15, 2023

Usifuate mkumbo..

Hakuna maisha yanayotesa watu kama ya mkumbo. Haya ni maisha unayopaswa kuyakataa. Ni maisha yaliyowapoteza wengi. Wapo walioona marafiki zao wanamiliki magari, wakaamua kukopa pesa na kwenda kununua magari. Baada ya muda mfupi, magari yakaharibika na wakajikuta wanaishi kwa shida kujificha huku wakiwa na madeni makubwa.

Unapaswa kujua kuwa, kila mmoja anayo riziki yake. Inapokuja hakuna anayeiondoa au kuirudisha nyuma. Kila mmoja namna anavyoishi anajua mwenyewe. Kupata kwake, kukosa kwake, anajua mwenyewe. Kitu kisichoonekana usoni mwetu ni matatizo, madeni, machungu na maumivu tuliyonayo. Siri ya moyo yetu aijuaye ni kifua. Mtu asipokwambia anayopitia, huwezi kujua.

Kuna wakati najiuliza kama ingetokea matatizo au nyakati ngumu tunazopitia au matendo tunayofanya yangejionyesha
usoni. Yaani unaona usoni mwa fulani mwizi, kahaba, mchezaji, msanii, tajiri, maskini, mchawi au mfukoni hana hata kumi. Hii ingekwa changamoto kubwa. Huenda tungeishi maisha yetu halisi kwa sababu hakuna anayeweza kufuata matendo mabaya yanayofanywa na mwenzake.  Inapotokea tumekosa, tusingeweza kuwatembelea ndugu au watu wa karibu maana wangejua kile tulichofanya.

Umemuibia mtu usiku akikutana na wewe mchana usoni mwako kunaonyesha kile ulichofanya. Anakukamata na kukuchukulia hatua. Lakini yote hayo hayajawa hivyo. Kila mmoja anajua namna anavyopata mahitaji yake.

Unachotakiwa ni kuishi maisha yako mwenyewe. Kama hujui mtu amepataje kitu, usilazimishe kuwa kama yeye. Huachi alama kwa kuishi kama fulani bali unaacha alama kuishi kama wewe. Fanya kile unachoona ni sahihi kwa ajili yako na jamii yako. Usifanye kwa ajili ya fulani. Hutoweza kupata furaha wala kutimiza lengo uliloweka kwa sababu hamasa
kiutendaji itakuwa ni ndogo. 

Wakati ndio huu kuweka mikakati mzuri juu ya kitu unachofanya ili baadaye uwe yule unayemtaka. 

Inawezekana sasa.

Imeandaliwa na Lackius Robert 
#20mwangaza2023

No comments:

Post a Comment