Monday, February 20, 2023

Usiangaike na maneno yao...

Kwenye maisha, watu wanayo nafasi ya kuamua kulingana na wanavyoona. Iwe ni sahihi au sio sahihi. Wanakuwa wanaamini wanachokisema kwa asilimia mia moja.

Inapotokea wewe ukawapinga inakuwa ngumu kukuelewe. Maana tayari kipo kitu wanakiamini kutoka kwao. Unachotakiwa kuzingatia ni yale unayoona yanafaa.

Ndio maana huwa ninasema mara zote wewe amua upande unaotaka. Maana ukifanya wanasema, usipofanya wanasema na ukiacha watasema pia. Pale unapoona panafaa ingia upande huo. Kisha fanya kinachowezekana kufanyika.

Wanakusema sio kwamba unakosea bali kuna hatua kubwa wanaona unaenda kuipiga. Hiyo, ndio inayowafanya wanakusema. Ukiweka nguvu kuyasikia maneno yao itakuwa ni ngumu kuendelea.

Hata wale walio karibu yako huwezi kuwazuia kusema. Nao watasema kulingana na namna wanavyoona inawafaa.

Wakati mwingine hata ukifa bado watasema kuwa fulani alikuwa hivi ama vile. Wajibu wako kama mtu unayetaka kufanikiwa kuweka nguvu kwenye kazi zako.

Huenda unajiuliza maswali, ufanye nini sasa?
Maana ukweli ndiyo huo kuwa, watu lazima watakusema iwe unafanya au hufanyi. Watasema bila kuwa na wasiwasi wowote.

Nakushauri, usiangaike na maneno ya watu juu yako. Usiangaike weka nguvu kwenye kazi zako. Fuata moyo wako kwa kile unachotaka kufanya. Pia, fuata ushauri huu wa aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Winston Churchill aliwahi kunukuliwa akisema,“Kwa muda mrefu Sasa nimeacha kuwasikiliza watu, badala yake naangalia kile wanachofanya. Tabia ndiyo ukweli pekee.”

Hutawazuia kusema ila unaweza kujizuia kufanyia kazi yale yasio mazuri kwako.

Imeandaliwa na Lackius Robert
0767702659

#25mwangaza2023

No comments:

Post a Comment