Tuesday, February 14, 2023

Jinsi kitabu cha Think and Grow Rich kilivyokuza shauku yangu

Mwaka 2019, wakati nafanya uchambuzi wa kitabu cha Think and Grow Rich chake Napoleon Hill nilipata mshangao mkubwa. Moja kati ya vitu alivyoandika ni shauku aliyokuwa nayo bwana mmoja Edwin C. Barnes. Bwana huyu alikuwa na shauku kubwa ya kuonana na kufanya biashara na  mgunduzi wa bulb za umeme Thomas Edison. Katika kitabu hicho mwandishi alijarbu kuonyesha namna gani mtu anavyokuwa na shauku na inavyomsaidia kufanikisha malengo na mipango yake. 

Anasema, akiwa anaelekea ofisini kwa Thomas Edison akili yake ilikuwa kazini. Alijihisi mwenyewe kama vile tayari alikuwa mbele ya Edison. Alisikia sauti ndani mwake ikimuomba Bwana Edison fursa ya kutekeleza jukumu zito katika maisha yake. Shauku yake ni kuwa mbia kibiashara na mgunduzi  huyu mkubwa. Alipofika mbele yake alikuwa na furaha kubwa na hapo aliona shauku yake imekuwa kweli. 

Miaka michache baadae alikuwa katika biashara na Edison. Shauku iliyokuwa imetawala katika maisha yake ilikuwa imegeuka kuwa kitu halisi.
Waliokuwa  wanamfahamu Barnes walianza kumuonea wivu kutokana na mafanikio aliyojaliwa maishani. Waliona katika siku zake za furaha, bila ya hata kujisumbua kuchunguza sababu za mafanikio yake.

Barnes alifanikiwa kwasababu alichagua lengo dhahiri, na akaelekezea kwalo nguvu zake zote. Matumaini yake yote pamoja na jitihada zake zote katika kulitimiza lengo hilo. Alikuwa yuko radhi kuanza na kazi ya chini kabisa, ilimradi tu kazi hiyo ingempatia japo fursa ya kupiga hatua moja kuelekea lengo alilokuwa amelipanga.

Ilikuchukua zaidi ya miaka mitano kabla hajafanikiwa kuipata nafasi aliyokuwa akiitafuta. Kwa kipindi chote hicho hakuwa na mwanga wowote wa matumaini, wala ahadi moja ya kufikiwa kwa shauku yake. Kwakuwa ni kitu kilichokuwa ndani ya moyo wake aliamua kujipa motisha mwenyewe. Katika akili yake alikuwa anajiona yupo mbele ya Edison kwa kila sekunde iliyokuwa ikipita. 

Kufanikisha lengo lake alitumia kauli isemayo “nitayaunguza madaraja yote nyuma yangu na kuweka rehani mustakabadhi wa maisha yangu na kupata ninachokitaka”  Alichokuwa anataka ni kuonana na kuingia ubia na Thomas na hilo ndilo wazo kuu alilokuwa awaza muda kwa mrefu.

Alipokuwa akienda kuonana naye hakusema, “nitajaribu kumshawishi Edison anipe kazi ya aina fulani”. Ila  “nikimuona nitampa ujumbe kuwa, nimekuja kuingia naye ubia wa biashara” hapa tayari alikuwa na mpango ulio tayari ni kitendo tu cha Thomas kuupitiana kufanya maamuzi. 

Hakusema, nitafanya kazi pale kwa miezi kadhaa ikiwa kama sitapata motisha, nitaacha na kutafuta kazi mahali pengine. Bali nitaanza popote, nitafanya chochote atakachoniambia nifanye. Ila ninachotaka ni kuwa mbia naye kibiashara na sio jambo lingine. 

Unaweza kuona namna gani ndugu yetu Barnes alivyokuwa amejipanga. Aliweka mipango sawa hakusubiri kufika kwa Thomas na kutafuta fursa. Bali alienda nayo kazi ibaki kwa Thomas kufanya maauzi. Alienda amedhamiria kufanya kila kitakachoweza kumkutanisha na Thomas ili mradi apate nafasi ya kuonana naye. Na hatimaye, alifanikiwa kupata kile alichokihitaji na kufanya kazi pamoja na Thomas. 

Barnes, hakuruhusu hali ya kutowezekana au hofu ndani yake. Unaweza kuona muda aliochukua hadi kufika mbele yake zaidi ya miaka mitano. Na hapo hakupewa hamasa wala neno la faraja kutoka kwa watu wengine. Badala yake walimuona kama mcheza sinema. Ila yeye pekee ndani yake ndiye aliyekuwa anajua ni nini anahitaji. 

Hapo ndipo tunaposema una machaguo mawili aidha ushinde au ufe. Kama vitani vile, ukiwa vitani hakuna kurudi nyuma. Huna cha barabara mbovu, maji mengi chakula hakuna au huoni mbele kazi ni moja tu upige au upigwe. Yote hiyo itategemea namna ulivyojipanga pamoja na shauku iliyo ndani yako. 

Shauku ni dira yako. Inatoka ndani yako kadiri unavyokuwa na shauku kubwa ndivyo unavyoyaandaa mafanikio makubwa ndani yako. 

Huwezi kuwa Barnes ila yapo masuala utajifunza na kuyafanyia kazi katika mambo yako ya kila siku. 

Kwa maelezo zaidi pitia uchambuzi wa kitabu hiki kwa kubonyeza hapa chini 


Imeandaliwa na Lackius Robert 0767702659 
#19mwangaza2023

No comments:

Post a Comment