Saturday, March 18, 2023

Usichoke, ndiyo maisha yetu


Kauli isemayo ukifaulu mtihani mmoja kwenye maisha usiwadharau waliofeli ni kweli kabisa. Kwa sababu maisha yanayo mitihani mingi sana. 

Unamaliza mmoja, unakuja mwingine zaidi yake. Unakumbuka siku umebanwa na kodi ya nyumba. Ukaumiza kichwa sana kuitafuta ili uendelee kulala chumbani kwako kwa raha mstarehe. Ile umemaliza kuilipa hivi, ukaambiwa mama anaumwa inatakiwa pesa ya matibabu. 

Ile furaha na amani uliyokuwa unaitegemea ilipotea ghafla. Pengine ukajisemea hii pesa inanipa furaha bandia. Nimekamilisha moja limekuja jingine. 

Umemaliza elimu ya chuo kikuu, ukiwa na dhana ya kwamba maisha umeyaweza. Hakuna kingine cha kukupa shida. Mara unakutana na janga la ukosefu wa ajira. Huu ni mtihani mwingine mkubwa. Unaanza kupigana nao. 

Umefanikiwa kuingia kwenye ndoa ukasema sasa mateso basi. Amani, furaha na starehe vinaanza. Majukumu yanapoanza kuwa mengi unajiuliza wapi pa kupumulia. Mke anataka hitaji hili, mtoto anataka hitaji lingine. Ndiyo maisha yetu. 

Pengine, umefanikiwa kununua gari ukasema; kuninginingia kwenye daladala basi. Ulipoipeleka garage gharama za vifaa na mafuta jasho linaanza kukutoka. Mawazo mengi juu ya services zake. Ndiyo maisha yetu ndugu. 

Sasa unafanya nini katika hali hiyo. Ni kitu kimoja unachohitaji na kitu hicho ni maandalizi. 

Uzuri wa kuwa na maandalizi katika kila kitu unachofanya yanakusaidia kupunguzwa uwezekano wa kushindwa. Ndio maana upo msemo wa wakati wa vita sio wakati wa kujiandaa. Bali kabla ya vita ndiyo wakati sahihi wa kujiandaa. 

Hata kwenye maisha yetu ndivyo ilivyo. Unahitaji kuwa na maandalizi ya kutosha kabla hujaanza kufanya kitu. Maisha yanatufundisha kila siku na mitihani tunayofanya ni majukumuku na kazi zetu za kila siku. 

Usiache kujiandaa na mambo yataenda vema. 

Una changamoto yoyote bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
Hamasika2023

No comments:

Post a Comment