Maono ni ile picha inayojengeka ndani ya mtu juu ya mambo fulani ayatarajiayo au yatarajiwayo kutokea katika uhalisia.
Maono haya mara nyingi hufananishwa na picha ya hitaji la mtu analotamani litimie. Mithali 29:18 inasema,
“Pasipo maono, watu huacha kujizuia; bali ana heri mtu
yule aishikaye sheria”.
Kwa maana nyingine ni kuwa, huwezi kufanikiwa katika maisha yako kama huna maono ya kile
unachotaka kupata katika maisha yako.
Tofauti kubwa iliiyopo kati ya watu waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa ipo kwenye maono.
Yaani, ile picha kubwa iliyo ndani mwao kuonyesha kule wanakotaka kwenda. Maono husaidia sana mtu kuweka nguvu kubwa ya kuzingatia kitu anachofanya.
Lengo lake kuu ni kuhakikisha hatoki kwenye uelekeo wake. Watu wenye mafanikio makubwa ni wale wenye maono makubwa na walio tayari kuhakikisha wanazingatia maono yao.
Ili na wewe uweze kuwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuzingatia, lazima uhakikishe unayaishi maono yako.
William Blake aliwahi kusema, “What is now proved was once only imagined.” Ikiwa na maana kama kitu kimepitishwa au kuhakikiwa basi kiliwahi kuwazwa.
Hapo unaweza kuona kwamba hakuna kitu kinachokuja bila kufikiriwa au kuwazwa. Hivyo, na wewe unapaswa kuwa na maono makubwa.
Angalia kitu unachofanya. Kisha angalia kwa miaka minne unataka uwe wapi? Hapo ndipo utaanza kutengeneza picha kubwa kwako. Hayo ndiyo maono unayotakiwa kuwa nayo. Unapokuwa umeweka maono unapaswa kujitoa kweli kweli.
Angalia aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee Nelson Mandela. Akafungwa miaka 27 gerezani. Ile picha aliyokuwa nayo hakuiacha aliisimamia vema. Hadi leo anakumbukwa kwa maono makubwa aliyokuwa nayo.
Wewe huwezi kuwa Mzee Mandela ila kuna kitu unaweza kufanya kupitia yale uliyojifunza kutoka kwake. Ijenge picha ndani yako ishi nayo uwapo katika utendaji wako, kisha ona uwezekano ndani yake.
Je, maono yako unayaonaje?
Bonga nasi hapa hapa 0767702659
Imeandaliwa na Lackius Robert
#34mwangaza2023
No comments:
Post a Comment