Monday, March 20, 2023

Ukifanya hiki utajitoa kwenye mazoea

Imekuwa kasumba kwa wengi wetu hasa mahali pa kazi kukwepa baadhi ya majukumu. 

Wakati mwingine unaenda katika ofisi fulani, ukitaka kupewa huduma fulani. Mhusika unayekutana naye, anakwambia nenda meza ile huyo atamaliza shida yako. 

 Unapochukua hatua ya kwenda kwa huyo mtu uliyeelekezwa labda ni IT au customer care badala amalizie shida yako anakwambia subiri kesho au kesho kutwa kuna mfumo haupo sawa. 

Pengine hamna shida yoyote, amejisikia uvivu tu. Hii hali imekuwa inarudisha nyuma maendeleo yetu kwa kiasi kikubwa. 

Unaenda kwa fundi anakwambia njoo baada ya siku mbili. Ukienda anakwambia umeme ulikata njoo keshokutwa. Ukija anakwambia kuna kifaa kakiagiza mahali. Huo wote ni uvivu tu wa kufanya kitu chako. 

Hii hali inapoendelea kuna watu wanaanza kujitoa taratibu taratibu kwenye biashara au huduma yako. Kwa sababu hakuna kitu wateja au watu wanakwepa kama kuzungushwa mara mbili au tatu. Ukimfanyia hivyo jua umempoteza. 

Ili tuwafanye wathamini huduma zetu, tuache uvivu kama kazi imekuja kwako ifanye kwa moyo wote. Muheshimu aliyeacha kazi zake akaja kwako umfanyie kazi. 

Kama ingekuwa halipi pesa yake sawa. Lakini wanalipa pesa ndicho kinachoumiza moyo. Pesa inatafutwa kwa shida. Hivyo, ukiiheshimu na ukaipokea kihalali watakuheshimu na kukupa kazi nyingi. 

Lijue hili likusaidie kukuza brand yako. Acha uvivu fanya kile kinachowezekana. 

Una changamoto yoyote bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert
Hamasika 2023

Saturday, March 18, 2023

Usichoke, ndiyo maisha yetu


Kauli isemayo ukifaulu mtihani mmoja kwenye maisha usiwadharau waliofeli ni kweli kabisa. Kwa sababu maisha yanayo mitihani mingi sana. 

Unamaliza mmoja, unakuja mwingine zaidi yake. Unakumbuka siku umebanwa na kodi ya nyumba. Ukaumiza kichwa sana kuitafuta ili uendelee kulala chumbani kwako kwa raha mstarehe. Ile umemaliza kuilipa hivi, ukaambiwa mama anaumwa inatakiwa pesa ya matibabu. 

Ile furaha na amani uliyokuwa unaitegemea ilipotea ghafla. Pengine ukajisemea hii pesa inanipa furaha bandia. Nimekamilisha moja limekuja jingine. 

Umemaliza elimu ya chuo kikuu, ukiwa na dhana ya kwamba maisha umeyaweza. Hakuna kingine cha kukupa shida. Mara unakutana na janga la ukosefu wa ajira. Huu ni mtihani mwingine mkubwa. Unaanza kupigana nao. 

Umefanikiwa kuingia kwenye ndoa ukasema sasa mateso basi. Amani, furaha na starehe vinaanza. Majukumu yanapoanza kuwa mengi unajiuliza wapi pa kupumulia. Mke anataka hitaji hili, mtoto anataka hitaji lingine. Ndiyo maisha yetu. 

Pengine, umefanikiwa kununua gari ukasema; kuninginingia kwenye daladala basi. Ulipoipeleka garage gharama za vifaa na mafuta jasho linaanza kukutoka. Mawazo mengi juu ya services zake. Ndiyo maisha yetu ndugu. 

Sasa unafanya nini katika hali hiyo. Ni kitu kimoja unachohitaji na kitu hicho ni maandalizi. 

Uzuri wa kuwa na maandalizi katika kila kitu unachofanya yanakusaidia kupunguzwa uwezekano wa kushindwa. Ndio maana upo msemo wa wakati wa vita sio wakati wa kujiandaa. Bali kabla ya vita ndiyo wakati sahihi wa kujiandaa. 

Hata kwenye maisha yetu ndivyo ilivyo. Unahitaji kuwa na maandalizi ya kutosha kabla hujaanza kufanya kitu. Maisha yanatufundisha kila siku na mitihani tunayofanya ni majukumuku na kazi zetu za kila siku. 

Usiache kujiandaa na mambo yataenda vema. 

Una changamoto yoyote bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
Hamasika2023

Friday, March 17, 2023

Nini kinafanya wakuchague?


Siku moja nilialikwa na taasisi moja kwa ajili ya kusimamia zoezi la usaili wa kazi. Kwenye jopo tulikuwa watu wanne . Kwa sababu mimi ni mtaalamu katika masuala la Sheria za Kazi na Ajira. Walinipa nafasi kubwa na wote walikuwa wanasikiliza neno la mwisho kutoka kwangu. 

Usaili kiukweli ulienda vizuri, nikiwa makini sana kuhakikisha anapatikana mtu sahihi. 

Wakati tunaendelea na usaili kuna dada mmoja tumuite Mwajuma japo sio jina lake halisi aliingia akaanza kujielezea background ya elimu na ujuzi wake. 

Kikafika kipindi cha maswali nikamuuliza swali la kwanza. Je, unajua nini kinafanya tukuchague wewe? 

Mwajuma akasema, ni Kwa sababu mkinichagua nitaweza kumsaidia baba yangu anayeumwa nyumbani. Matibabu yatatokana na mshahara mtakaonilipa. 

Nilimwambia tumekusikia. Nikashika kichwa na kujiuliza maswali mengi. Je, huyu anajua anachofanya? Na hiki alichosema anakijua au amesahahu kwamba  hakuna mtu anayekupa kazi kama msaada. 

Baadaye wakata tutoe hitimisho juu ya usaili mzima. Binafsi nilimwambia bosi kwamba mtu pekee mwenye sifa alikuwa ni mmoja tu Mwajuma. Ila tatizo ni moja. Ajajua ni kwa nini anatafuta kazi. 

Kwa hiyo either mtangaze upya au mchukue Mwajuma kisha muelekeze namna bora ya kufanya kazi. Mwambie hupewi kazi kwa sababu ya matatizo uliyo nayo au kama msaada bali ujuzi na namna unavyoweza kuisaidia taasisi kuzalisha zaidi. 

Note: Ukiwa unaomba kazi mahali popote pale, elezea namna utakavyofanya kazi hiyo kwa ufanisi, uadilifu na faida utakayoongeza. Na sio unavyotaka kutatua matatizo yako kupitia kazi.

Usiseme  nina mtoto mdogo na hakuna wa kunisaidia. Ninataka kujikimu kimaisha. Baba yangu anaumwa au mama yangu au kwa sababu nipo tu nyumbani.

Waambie ninaweza kufanya 1, 2, 3 na nipo tayari kufanya kazi kwa jitihada zote ili kuhakikisha kampuni au biashara hii inafikia hatua nzuri.

Sehemu nyingi za kazi wanatafuta wafanyakazi wanaoenda kuleta suluhu na sio kuongeza matatizo. Ikiwa umepata nafasi, usiichezee tena umefika kwenye usaili wa kuongea. Hupaswi kutia doa. 

Funguka onyesha ujuzi wako, hadi wanaofanya usaili washangae. Hii itafanya waone kitu cha ziada kwako. 

Waonyeshe namna unavyoenda kukuza uzalishaji katika kampuni au taasisi husika. Itakutofautisha na wengine. 

Umewahi kukataliwa mahali kisa huna vigezo, ulijua kwa nini? 
Bonga nasi hapa hapa 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
Hamasikaacademy2023

Thursday, March 16, 2023

Nguvu ya jina la kwanza

Helow! Robert, habari yako? 
Helow Lackius, habari yako? 

Hawa ni watu wawili tofauti wanaopiga simu kwa wakati tofauti. Ila attention inachukuliwa na kwa mtu wa pili. Unataka kujua kwa nini? 

Kuna nguvu kubwa ya kutaja jina la kwanza la mtu. Inaonyesha kabisa unamfahamu. Hata kama umepewa namba na mtu ila akakupatia majina mawili, ukitaja jina lake la kwanza. Kuna umakini mkubwa unautengeneza kwake. Mtu aliyepigiwa anaitwa Lackius Robert. 

Ipo hivi sauti ambayo mtu anapenda kuisikia mara nyingi ni jina lake. Hata kama yupo sehemu yenye kelele kubwa, ila akisikia jina lake lazima aweke umakini mkubwa. Hii ni kwa sababu ndiyo sauti anayopenda kusikia. 

Unapokuwa umetaja jina la pili, anakuwa na wasiwasi ikiwa unamjua vema. Anaweza kuhisi kuna umakini fulani unaukosa. Sio kwamba hawezi kuendelea kukusikiliza ila unapokuwa umetaja jina la kwanza anaongeza umakini mkubwa. 

Ukitaka kujua hili, piga simu kwa mtu uliyepewa namba yake akiwa mpya. Anza kutaja jina lake la kwanza utaona namna atakavyoruhusu mazungumzo yenu. 

Wewe timiza hili, taja jina lake la kwanza mara zote unapoongea na mtu. Iwe ni mteja, rafiki au mtu mwingine, usiache kumuita jina lake la kwanza. Ndio siri kubwa iliyofichwa kwenye jina la kwanza. 

Kingine cha kuzingatia ni kutaja jina lake kwa ufasaha zaidi. Epuka kukosea jina la mtu wakati wa kulitaja. Mfano anaitwa Lackius. Epuka kutumia Lackilius utaondoa umakini wake ataona ujali na huna umakini hata kidogo. 

Unapata changamoto yoyoye bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
Mwangaza 2023

Monday, March 13, 2023

Unaweza kushinda mchezo wowote

Napoleon Hill kwenye kitabu chake cha "Think and Grow Rich" anasema "washindi kwamwe hawaachi kufanya". 

Hii kauli inatosha kukupa nguvu na imani kuwa unaweza kuwa mshindi katika mchezo wowote. Iwe mpira, biashara, muziki au kitu kingine. 

Ikiwa unacheza mpira, kama utaendelea kufanya mazoezi bila kuacha. Kujifunza mbinu mpya na kuwa na nidhamu bora hakuna namna utashindwa kufunga magoli mengi zaidi. 

Upo kwenye biashara, ushindi wako ni mauzo. Maana kupitia mauzo ndipo pesa hupatikana. Ushindi huo unaenda kuupata pale ambapo utaamua kufanya endelevu bila kuacha. Unajifunza mbinu mpya za masoko kila siku. Hapo lazima uuze na mchezo wa mauzo kwako itakuwa raha maana utakuwa ni mshindi. 

Upo kazini, ikiwa utaonyesha kujali, kujituma, kuwa na nidhamu na kumaliza kazi kwa wakati. Lazima uwe mshindi katika kazi zako. Maana kupitia nidhamu utajiboresha na kukamilisha kazi zako kwa muda muafaka. 

Ushindi ninaozungumza hapa sio tu wa goli kusema wachezaji ndio wanaostahili kushinda la asha! Ni ushindi katika kazi zako. 

Hawajibu message piga simu. Hawajapokea simu watembelee. Mara zote hakikisha kuna kitu kikubwa unakifanya ukilinganisha na hapo awali. 

Mwanamziki piga kazi zaidi. Jifunze na andaa muziki wenye maadili ili watu wote waweze kupata ujumbe. Kuwa mvumilivu usikate tamaa haraka sana. Ushindi kwenye mziki ni wako. Endelea kuonyesha juhudi kubwa. 

Changamoto ni nyingi tunapitia, wewe fanya tu, timiza wajibu wako kufanya. Kama ni simu 20 wewe piga, kama ni kuwatembelea watu 10 kwa siku ili uwauzie wewe nenda. Kama ni mazoezi wewe nenda. 

Hakikisha mara zote, unakuwa kazini. Fanya bila kuchoka. Unaambiwa mchumia juani ulia kivulini. Wakati ndio huu ushindi wako unakaribia. Kila lakheri.

Je, ni nini kinakukwamisha  ushindi wako kwenye kazi zako? 

Bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
Karibu sana tujifunze zaidi. 

Saturday, March 11, 2023

Mabadiliko yanaanza na wewe


Kama kitu kimetengenezwa kinaweza kubadilishwa. Kama kitu kina uhai kinaweza kubadilika kwa hali fulani fulani. 

Chukulia mtoto mdogo anapozaliwa, haanzi kuongea, kutembea au kuwa na meno. Kadiri muda unavyokuwa unasogea ndivyo anavyokuwa anabadilika mdogo mdogo. 

Chukulia mti wa Mbuyu, mwanzoni huwa unaanza kama mchicha. Wakati huo umbo likiwa dogo sana kadiri muda unavyokuwa usogea ndivyo hubadilika pia. Hadi kuwa na umbo kubwa. Ukiambiwa ulikuwa katika umbo dogo unaweza usikubali lakini huo ndio ukweli. 

Ipo hivyo kwenye maisha yako. Hutaweza kubadili mwili au kujiongezea kiungo kingine kwa maana ya mkono wa watatu au mguu wa tatu la asha! Namaanisha unaweza kuibadili hali ya sasa kuwa bora zaidi. 

Huwezi kuibadili jana ila unaweza kuitumia leo kuiboresha kesho yako. Mabadiliko yote haya yanaanza na wewe mwenyewe. Kukubali kuwa kuna mahali unataka kufika. Kuna kitu unataka kukipata katika maisha yako. Kuna hatua kubwa unataka kuipiga. 

Huo ndio ukweli ninaotaka uweze kuujua "any changes starts with you" mabadiliko yoyote yanaanza na wewe. 

Unataka kubadilika kifikra, kimawazo, kimtazamo na kihisia pia. Hii itakusaidia kuwa tayari kutimiza wajibu wako. Kumaliza kile ulichokianza, bila kujali ugumu kiasi gani unapitia. 

Matumaini unayotaka kuwa nayo. Kuwa tayari kupata habari zaidi. Usipoamua kufanya kitu tambua kuwa wewe ndiye muongozaji katika njia yako. Mafanikio unayotaka yanaanzia kwenye akili yako. Unapaswa kuwa tayari kubadilika kimwili na kiroho pia. 

Ni mengi unahitaji kufanya, wakati ndio huu kuyafanya. Hakuna wa kukuzuia kuyafanya. Ni wewe tu kukubali kubadilika na mabadiliko ya kweli unayotakiwa kuyapata yaanzie akilini mwako. Namna unavyoishi kuwa mtu mwenye focus, weka lengo kutimiza malengo. 

Hiyo yote ukiifanikisha amini maisha yako yatabadilika. Usijali kuhusu muda. Wewe jali juhudi unazoweka kuendana na mabadiliko hayo. 

Kumbuka, Umri sio shida. Kipato chako, mahali unapoishi vyote hivyo havina shida. Ukitaka kubadili chochote anza na wewe. Usikimbilie kutoa lawama kwa watu. Huenda walichangia kuanguka kwako lakini hiyo haiwezi kukuzuia kupata unachotaka.Badilisha mawazo na akili yako na kufanya kile kilicho sahihi. Hakika utafanikiwa. 

Je, ni kitu gani kinakuzuia kuendana na mabadiliko? 

Bonga nasi hapa hapa 0767702659 
Imeandaliwa na Lackius Robert 

Wednesday, March 08, 2023

Ni kidogo lakini kinampa faraja

Kila kuna kitu kinampa nguvu kubwa hasa pale anapofanyiwa kitu kizuri. Iwe ni pesa amepewa au hamasa amepata. Kutokana na faraja baada ya kupitia hali fulani nzuri au ngumu. 

Ninapoona sentensi hii napata faraja sana "With people, little things are the big things" ikiwa ina maana ya vitu vidogo, kwa watu vina nguvu sana. 

Ila umfanye mtu ajisikie vizuri huna haja ya kumpa zawadi ya gari, pesa nyingi au kumpatia nyumba. Au iwe na elimu ya juu. Ni kupitia vitu vidogo unavyomfanyia ndivyo humfanya mtu ajisikie vizuri. 

Huenda unajiuliza ufanye vitu gani ili umfanye mtu ajisikie vizuri. Jibu hili hapa. 

Unahitaji kutoa kitu kidogo kinachotoka moyoni mwako. Mfano mtu anaumwa ukaenda kumjulia hali anafurahi. Unamtumia ujumbe au unampigia simu ya kumpa pole. Unamtembelea, huna kitu lakini uwepo wako unampa nguvu kubwa sana. 

Mama amejifungua, umeenda kumjulia hali na zawadi kidogo kwa mtoto. Ni faraja tosha kwa mama mzazi. Sio mpaka uwe na pesa nyingi au ndo uende kumuona. Ujio wako unamfanya ajisikie vizuri. 

Mtu kafiwa na mpendwa wake sio mpaka uwe na vitu vingi kwenda kumfariji au una kiasi kingi  cha pesa nenda. Nenda na hicho kitu kidogo. Kaa naye mfariji mpe pole inamfanya ajisikie vizuri. 

Kwa bahati mbaya walio wengi wetu wanachofanya ni kusubiri wawe na vitu vingi. Kama ni pesa ziwepo nyingi. Kama ni mali au vitu awe na vitu vingi kama vyakula au vitu vingine. 

Ukweli ni kuwa, chochote  kidogo ulichonacho na ukakitoa kwa moyo wako wote kinamfanya ajisikie vizuri. 

Unachotakiwa ni kufanya kile kinachowezekana kwako. Usimpe mtu ukabaki na kinyogo moyoni. Toa kidogo, lakini moyoni ufurahie au ubaki na amani moyoni. 

Hii ndio siri kubwa ya kumfanya mtu ajisikie vizuri. Toa kitu ata kama ni kidogo, ila ukiwa na kitu kikubwa usiache kutoa kikubwa kisa umeambiwa toa kidogo. 

Je, wewe uliwahi kufanyiwa kitu kipi kikakufurahia? 
Bonga nasi hapa hapa 0767702659. 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
#37mwangaza2023

Tuesday, March 07, 2023

Hiki ndicho huvunja uaminifu

Ni matumaini yangu kuwa umewahi kusikia watu wakisema fulani kanichomesha mahidi au kaniacha njia panda na maneno mengine. 

Kanipa ahadi hafu kashindwa kuitimiza. Ni hali ambayo inamfanya mtu anakasirika sana. Na mwanzo mpya wa kutopokea simu ya mtu au kukata mawasiliano. 

Huenda imewahi kukutokea au haijawahi kukutokea. Ila ukweli ninaotaka uujue leo ni kuwa: hakuna kitu kinavunja uaminifu kwa mtu kama kutotimiza ahadi. 

Kuweka ahadi ni rahisi ila kazi ipo kwenye kuitimiza. Unapoweka ahadi na mtu, iwe ya pesa au zawadi, jua kuna umakini unautengeneza kwa mtu. 

Kama ni pesa ahadi yako inamfanya aweke mipango juu ya pesa hiyo. Inapotokea hujaweza kutumiza ahadi hiyo lazima mgombane. 

Kuna kitu kinapungua ndani yake ambacho ni uaminifu. Namna ambavyo alikuwa ana imani juu yako anapunguza. 

Ninaposema ahadi sio tu kwenye pesa ata maeneo mengine. Wewe kiongozi umeahidi kutekeleza vitu fulani ndani ya uongozi wako. Muda Miaka mitano inapoisha hujatekeleza. Jua kuna kitu unakipunguza kwa watu wako ambacho ni uaminifu. 

Unahitaji nini ili kutimiza ahadi? Kitu unachopaswa kujua ni kwamba. Sio usome masomo ya juu au usome vitabu 100. Unachohitaji ni uwezo wa kufikiri kilichosahihi kwa wakati sahihi. Usitoe ahadi ukiwa na FURAHA sana au UMEKASIRIKA sana. Toa ahadi ukiwa katika hali yako ya kawaida. 

Kingine, toa ahadi iliyo ndani ya uwezo wako. Epuka kutoa ahadi kwa sifa. Upo mbele za watu au kwenye harusi. Unataka watu wakuone baba la bab au mama la mama itagharimu. 

Weka ahadi iliyo ndani ya uwezo wako. Hii itakusaidia kuitimiza bila kuwa na wasiwasi. Watu wengi huweka ahadi ili wasifiwe inapofika kwenye kuitekeleza ndipo shida huanzia.

Ahadi haipaswi kuwa ile ya kukufanya ukose amani. Inapaswa kukupa hamasa kutafuta zaidi. Weka akilini kuwa, kinachovunja uaminifu ni ahadi hewa. Take care uutunze na kuulinda uaminifu. 

Je, ahadi ipi uliahidi na hukutimiza? 
Bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
#36mwangaza2023

Monday, March 06, 2023

Uwezo wako wa ushawishi umefichwa huku

Kila mtu anao uwezo ndani yake. Uwezo kwa kumshawishi mtu kuchukua hatua. Katika hili, wapo wanaopata uwezo huu kupitia nafasi zao za uongozi au shuleni. Huku wengine wakiupata kutokana na uzoefu katika kufanya vitu tofauti. 

Ipo njia pekee inayoweza kutumiwa na wote, bila kujali elimu, jinsia wala dini. Na njia hii ni kuwa na shauku kubwa ndani yako. Namna ambavyo unaongea na mtu yeyote kuna kitu anakiona ndani yako. Iwe upole, utii, utukutu au utulivu. 

Ninaposema kuwa na shauku kubwa maana yake ni kwamba; namna unavyoongea na mtu unamfanya awe na umakini kwa sababu kile unachoongea unamaanisha. 

Mtu mwenye shauku anakubaliwa kwa watu wengi. Ipo hivi, tupo kwenye dunia yenye changamoto kila uchao. Watu wengi wanahitaji kupata faraja kutoka kwako. Mfanye kila unayekutana naye afurahi. Na hii itatokana na shauku kubwa iliyo ndani yako. 

Mtu mwenye shauku haogopi, anakuwa na hamasa wakati wote. Anakuwa na uso wa furaha. Sauti anayoitamka inakuwa inatoka vizuri na kusikika tofauti na asiye na shauku. 

Hii ndiyo nguvu kubwa iliyo ndani yako. Mwenye shauku kubwa ya kufanya hakatishwi tamaa na hali anazokutana nazo wala changamoto. Anakuwa na imani kubwa ndani yake. Anapenda wale wanaokutana naye wafurahi zaidi. 

Mmoja kati ya watu waliokuwa na shauku kubwa katika utendaji wao alikuwa Mery Teresa(Mother Teresa) mwanzilishi wa "Mission Of Charity" . Alisifika kuwa na shauku kubwa kuwasaidia watu wanaotoka katika familia masikini. Hii ilifanya dunia itambue mchango wake. 

Haikuishia hapo alipewa tuzo ya Nobel kwa usisitizaji wa upendo kwa watu wanaotoka katika familia za chini. Alikuwa mtetezi wa haki zao. Alipofaliki kanisa katoriki waliamua kuenzi mchango wake kwa kumuita mtakatifu ndipo jina la Mother Tereza likapatikana. 

Moja kati ya misemo yake ilikuwa "The fruit of silence is PRAYER. The fruit of prayer is FAITH. The fruit of faith is LOVE. The fruit of love is SERVICE. The fruit of service is PEACE". Ikiwa na maana, "matunda ya ukimya ni maombi. Matunda ya maombi ni imani. Matunda ya imani ni upendo. Matunda ya upendo ni huduma. Matunda ya huduma ni amani". 

Ukiwa na shauku kubwa ya kufanya vema kitu unachokitaka dunia itaona na watathamini mchango wako. Shauku ni ile nia ya kufanya kitu iliyo ndani yako. Msemo mwingine aliowahi kusema Mother Tereza ni "ishi kama mnyama kufa kama malaika". Akimaanisha fanya kazi yako kama mnyama maana mnyama huwa anasukumwa anapigwa ili kazi fulani zikamilike na huwa hachoki. 

Uwezo wake wa ndani ulidhihirishwa na shauku kubwa. Ile nia na upendo aliokuwa nao kuwasaidia watu masikini. Mchango wake utaenziwa daima na milele. 

Huwezi kuwa kama Mother Teresa ila kupitia yeye kipo kitu unaweza kufanya. Ionyeshe dunia shauku iliyo ndani yako na wafanye walio karibu yako kufurahia uwepo wako. Na mungu atakubariki. 

Je, uwezo wako unafichwa katika kitu kipi? 
Bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
#35mwangaza2023

Sunday, March 05, 2023

Maono na uwezekano

Maono ni ile picha inayojengeka ndani ya mtu juu ya mambo fulani ayatarajiayo au yatarajiwayo kutokea katika uhalisia. 

Maono haya mara nyingi hufananishwa na picha ya hitaji la mtu analotamani litimie. Mithali 29:18 inasema,
“Pasipo maono, watu huacha kujizuia; bali ana heri mtu
yule aishikaye sheria”. 

Kwa maana nyingine ni kuwa, huwezi kufanikiwa katika maisha yako kama huna maono ya kile
unachotaka kupata katika maisha yako. 

Tofauti kubwa iliiyopo kati ya watu waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa ipo kwenye maono. 

Yaani, ile picha kubwa iliyo ndani mwao kuonyesha kule wanakotaka kwenda. Maono husaidia sana mtu kuweka nguvu kubwa ya kuzingatia kitu anachofanya. 

Lengo lake kuu ni kuhakikisha hatoki kwenye uelekeo wake. Watu wenye mafanikio makubwa ni wale wenye maono makubwa na walio tayari kuhakikisha wanazingatia maono yao. 

Ili na wewe uweze kuwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuzingatia, lazima uhakikishe unayaishi maono yako.

 William Blake aliwahi kusema, “What is now proved was once only imagined.” Ikiwa na maana kama kitu kimepitishwa au kuhakikiwa basi kiliwahi kuwazwa. 

Hapo unaweza kuona kwamba hakuna kitu kinachokuja bila kufikiriwa au kuwazwa. Hivyo, na wewe unapaswa kuwa na maono makubwa. 

Angalia kitu unachofanya. Kisha angalia kwa miaka minne unataka uwe wapi? Hapo ndipo utaanza kutengeneza picha kubwa kwako. Hayo ndiyo maono unayotakiwa kuwa nayo. Unapokuwa umeweka maono unapaswa kujitoa kweli kweli. 

Angalia aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee Nelson Mandela. Akafungwa miaka 27 gerezani. Ile picha aliyokuwa nayo hakuiacha aliisimamia vema. Hadi leo anakumbukwa kwa maono makubwa aliyokuwa nayo. 

Wewe huwezi kuwa Mzee Mandela ila kuna kitu unaweza kufanya kupitia yale uliyojifunza kutoka kwake. Ijenge picha ndani yako ishi nayo uwapo katika utendaji wako, kisha ona uwezekano ndani yake. 

Je, maono yako unayaonaje? 

Bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
#34mwangaza2023

Saturday, March 04, 2023

Hii ndiyo sababu inayofanya usahau ulichojifunza

Mara ngapi umekuwa unajifunza vitu vingi na kutofanyia kazi hata kimoja? 

Unakumbuka ile siku uliyomaliza kusoma kitabu fulani? Ule mzuka uliotoka nao ukasema nitaenda kufanyia kazi kile ulichojifunza. Ila baada ya siku kadhaa kupita hakuna kilichofanyika. 

Au ulipotoka kwenye semina ya biashara, uongozi, mahusiano au ndoa. Uliwahakikishia watu kuwa unaenda kufanya mabadiliko makubwa sio tu katika kazi zako bali katika maisha yako. 

Kila walipokuuliza uliwaambia umejifunza mambo mengi sana, kiasi kwamba unaenda kufanya maajabu makubwa. Mwezi mmoja mbele hamna kilichofanyika. Umesahau kila kitu. Unataka kujua tatizo ni nini? 

Ipo hivi "To know and not to do, is really not to know. To learn and not to do is not to learn". Kwa lugha nyepesi; kujua kitu na kutokifanya ni sawa na kutokijua. Kujifunza kitu na kutokifanyia kazi ni sawa na kutojifunza. 

Huu ndio ukweli. Unaweza kujifunza vitu vingi lakini ukachagua vile vichache vya kufanyia kazi. Mfano unaposoma kitabu usijipe presha et hadi ufanyie kila kitu. Chagua vitu vichache vya kufanyia kazi. 

Umehudhuria semina, umejifunza mengi. Huwezi kuyafanyia kazi yote chagua machache ya msingi. Umejifunza kuwa, ili uweze kuwa mwekezaji lazima utunze asilimia 30 ya kipato chako, asilimia 10 ya zaka au kumshukuru Mungu. Asilimia 10 msaada au asilimia 50 ya matumizi kwa mfano. Huwezi kuanza vyote kwa pamoja. 

Anza kidogo kidogo na kitu kimoja. Ili baadaye uanze kuzoea. Ila usipofanyia kazi vitu vyote. Jua ni sawa na kutojifunza. Utaelewa zaidi baada ya kuanza kufanyia kazi kitu. 

Mmejifunza biashara. Ili upate ufahamu mzuri wa biashara, fungua biashara. Hapo ndipo utaanza kuona namna gani mambo yanavyoenda na hapo ndipo utapima ubora na uelewa wako, kuhusu mliyojifunza. 

Kila siku, jifunze kitu na ujenge utamaduni wa kufanyia kazi machache uliyojifunza. Itakusaidia kwa kiasi kikubwa kuelewa na kukumbuka zaidi. Ndiyo maana unasahau kile ulichojifunza kwa sababu hufanyii kazi kitu hicho.

Je, ni nini kinakukwamisha kufanyia kazi uliyojifunza? 

Bonga nasi 0767702659 
Lackius Robert 
#33mwangaza2023

Friday, March 03, 2023

Tushirikiane sisi ni wamoja

Nilipata hamasa zaidi niliposoma hadithi inayosema kuwa:

"Kwenye Shule moja kulikuwa na kundi la wanafunzi watukutu ambao walikuwa wakionea wanafunzi wenzao. Wanafunzi hao walikuwa wakikuta mwanafunzi mwingine wanamlazimisha achague wa kupigana naye na akikataa wanampiga wote.

Siku moja kundi hili walikutana na mwanafunzi mmoja aliyeonekana kuwa mnyonge sana. Wakamwambia achague wa kupigana naye. Yule mwanafunzi akachora mstari na kusema yule ambaye anajiona ndio mbabe kuliko wote avuke huu mstari. Yule ambaye ndio alikuwa mbabe alivuka mstari ule na alipofika upande wa pili yule mwanafunzi mnyonge alimwambia sasa tupo upande mmoja, tuungane kupambana na hao wengine. Yule mbabe akakubali wakaliamsha kuwapiga wengine".

Unaweza kuona ni usaliti lakini sio kweli huyu mnyonge alimwambia neno la msingi. Huenda mtoto mbabe hakuwahi kulisikia. Maisha yeke yote aliishi kupigana na kushindana. Lakini alipoambiwa "tupo upande mmoja, hivyo tuungane pamoja". Aliona kuna jambo la msingi.

Hata maisha yetu ndivyo yalivyo. Mnapokuwa upande mmoja mnapaswa kuwa wamoja. Kushirikiana, kushauriana na kushirikishana katika masuala mbalimbali ya maendeleo.Bila kusahau watu wote wanaokuzunguka. Hao mpo nao upande mmoja. Ni vema kusaidiana na kushirikishana. 

Tatizo ni kwamba wengi wetu hatuelewi hii dhana ya umoja. Ndio maana tumekuwa tunashindana lakini hatufiki mbali.

Mfano. Kama wanandoa wangejua kwamba wapo upande mmoja, wa kutaka maisha yao wote kuwa bora basi matatizo mengi sana ya ndoa yasingekuwepo na ndoa zingedumu. Lakini baadhi ya familia, unakuta mme anashindana na mke wake. Wakati mwingine mke anamuibia mali mme wake. Inashangaza sana.

Mwajiri na mwajiriwa hawa wote wapo upande mmoja. Kila mmoja yupo kunufaisha kazi yao na maisha yao kwa ujumla. Lakini mambo ni tofauti huyu anamkwaza na kumkandamiza mwenzake mara anamuibia. Vitu vya kushangaza vinafanyika.

Nashangaa kwanini  tunafikiri kwamba tuko pande tofauti na hivyo kuishia kushindana, mashindano ambayo hayamfaidishi hata mmoja wetu. Mke na mme kushindana, kuibiana. Mtu na mdogo wake kunyanyasana, kutesana na kuibiana. Inashangaza sana.

Wakati ndio huu. Tushirikiane sisi ni wamoja. Tuache ushindani. Baba na mama jenga familia bora. Mwajiri na mwajiriwa ikuze taasisi yenu kupitia umoja. Hakika mtafanikiwa.

Je, nini kinazuia maendeleo yako?

Bonga nasi 0767702659
Imeandaliwa na Lackius Robert
#33mwangaza2023

Thursday, March 02, 2023

Jifunze Ushirikishe

Ukweli ni kuwa kila mmoja wetu kipo kitu anakijua zaidi wengine. Huenda ni upande wa hesabu, lugha, fedha, uongozi, mahusiano au biashara. 

Kila wakati umekuwa mstari wa mbele kujifunza vitu vipya. Lakini cha kushangaza kuna baadhi ya vitu umekuwa ukivisahau. Hali inayokufanya kurudia kuvisoma tena ili vikae. 

Hali hii ya kuwa unasahau kuna wakati imekuwa ikikunyima furaha. Kwa sababu muda ambao ungefanya kitu kingine unautumia tena kupitia. 

Umekuwa unajiuliza namna ipi nzuri kujenga kumbukumbu ya muda mrefu. Njia hii hapa "jifunze shirikisha". 

Ipo hivi "you learn best when you teach another" kwa lugha nyepesi. Unajifunza kuwa bora kupitia kufundisha wengine. Hii ndiyo siri ninayokupa leo. 

Unasoma masuala ya ndoa. Unasoma makala na vitabu vya ujasiriamali, sanaa, biashara au uongozi. Tafuta sehemu au watu wa kushirikisha maarifa yako. 

Inaweza kuwa katika mitandao ya kijamii kama Facebook, Whatsapp, linked au telegram. Au ukaamua kuandika kitabu au jarida, linaloelezea masuala mbalimbali unayojua. 

Uzuri wa kushirikisha ni kwamba unapata uelewa zaidi. Tunasema unachomfundisha mtu kinanasa haraka akilini kuliko kile usichoshirikisha. 

Jifanyie tathmini. Hata kama ni vitu vya kawaida kama kumfundisha mtu kutumia simu, kupika chakula fulani. Namna unavyokumbula hatua zote. Na pengine unahisi kama yule uliyekuwa unamfundisha upo unamuona mbele yako. 

Wenye uwezo mzuri wa kutunza kumbukumbu hawajashushwa kama ulivyokuwa unadhania. Walichukua wajibu kujifunza na kushirikisha yale wanayojua. 

Wakati ndio huu. Ifanye dunia ijue kile kilichomo ndani yako. Ili baadaye uwe na uwezo mkubwa kuwa na kumbukumbu nzuri. 

Je, nini kilikuwa kinakukwamisha kuweka kumbukumbu zako? 

Bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
#32mwangaza2023

Wednesday, March 01, 2023

Fanya kinachowezekana

Ni mara nyingi tumekuwa tunaacha kufanya baadhi ya vitu kwa kujipa moyo kuwa ni vigumu kufanyika. Unakuta mtu anafanya kitu kwa muda mchache anaacha kisa kuna ugumu anauona au kukutana nao. 

Lakini ukweli ndio huu kwamba vitu vingi, ili vikamilike kuna juhudi nyingi zinapaswa kutumika. Juhudi hizi zinapaswa kuwa endelevu zaidi ya kawaida. Sasa wengi wetu baada ya kuona juhudi nyingi tunazoweka bila kupata matokeo huwa tunakata tamaa. 

Hali inayofanya tushindwe kabisa kufanya vitu. Na pengine kuamua kufanya vitu vingine vipya zaidi tukihisi vitu vya kwanza havijafanya kazi. Leo ipo njia pekee nimekuletea nakushauri uifanyie kazi.  Sio njia ambayo ni nyepesi kufanya ila ukiifanya kuna kitu kinaweza kuongezeka au ufanisi fulani katika kazi zako. Njia hii ni hii hapa. 

Fanya kinachowezekana. 

Hii ni njia na msemo unaoweza kuutumia kila siku katika maisha yako na utendaji wako. Kabla hujaacha kitu na kuanza kingine hakikisha kitu kimefanyika au jambo limefanyika. Umepanga kitu kabla hujakifanya unaachia njiani nakushauri kuitumia njia hii. Wewe fanya kile kinachowezekana. 

Ni binti unahitaji kuzungumza naye kabla hujaacha fanya kitu. Usijipe majibu. 
Kwa taarifa yako hakuna vitu au biashara inayoanza ikiwa kubwa wala mafanikio yanayoanzia juu. Vyote vinaanzia katika hatua za awali. Ikiwa na maana ya wahusika kufanya kile kinachowezekana. 

Unataka kufungua duka. Fungua kisha unanze kuuza kadri utakavyoweza. Fanya kinachowezekana kufanyika. Usishindane na watu. Wewe fanya kilicho ndani ya uwezo wako wote. Hii itakusaidia kuona wapi panahitaji maboresho au kufanyiwa kazi zaidi. 

Uzuri wa kufanya kinachowezekana ni kwamba unapata nguvu ya kuendelea zaidi. 

Kila mara kabla hujaacha kitu jiulize je, nimefanya? 
Kisha rudi kwenye msingi wa kufanya kinachowezekana kufanyika. Wasiliana nasi 0767702659.

Imeandaliwa na Lackius Robert 
#32mwangaza2023