Tuesday, August 27, 2024

Fanya Kazi Kwa Ubora, Matokeo Yatakulipa Yenyewe

Ndugu, 
Karibu katika mwendelezo wa masomo yetu hapa.

Leo tutajifunza namna gani unaweza kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu ili kujiweka karibu na wateja wako. Tutaanza na simulizi, kisha tutaangalia hatua za kuchukua.

"Ilikuwepo kampuni moja ya uuzaji wa magari, katika kampuni ile, alikuwepo dereva hodari ambaye alisifika kwa kuendesha vema na kuwasimia vema madereva wengine.

Dereva huyo alifanya kazi kwa muda mrefu sana katika kampuni ile. Katika nyakati tofauti tofauti alihitaji kuongezewa mshahara, lakini bosi wake alionekana kama
vile hajali kabisa na hana mpango wa kumwongezea mshahara hadi ulipobakia mwezi mmoja kwa yeye kustaafu.
Kabla ya muda kufika, Mkurugenzi alimwita dereva Juma na
kumwambia kuwa kuna tenda imepatikana ya kuuza gari, naye angependa ampe hiyo tenda
aisimamie iwe ndio kazi yake ya mwisho katika kampuni ambayo pia ingeacha alama yake.

Dereva Juma alikubali kwa shingo upande na akawa analalamika kwa kila mtu pale ofisini kuwa bosi wake hana utu na anaendelea
kumfanyisha kazi bila hata kumwongezea mshahara kama alivyomwomba.
Basi, alienda kuchagua gari zinazoweza kuwa imara kwa ajili ya kuziuza. Kwa kuwa alikuwa ameshavunjika moyo, hakutafuta gari imara, ili amkomoe mkurugenzi washindwe tenda hiyo.
Dereva Juma akawasiliana na 
mkurugenzi kuwa gari la sample limepatikana na atapita juu kwa juu kwenda kwenye sehemu husika waliyotangaza tenda. 
Dereva Juma alipofika sehemu husika, alishangaa kumuona Mkurugenzi na wafanyakazi wenzake na sio wateja kama alivyofikiri.
Dereva Juma akafika, akashangaa watu wanashangilia gafla Mkurugenzi akaja na kumwambia Dereva Juma; Kuanzia sasa hii gari ni yako, ni shukrani yangu kwa muda wote ambao umefanya kazi katika kampuni yetu.
Wakati wafanyakazi wanashangilia yeye alianza kulia. Kilichofanya alie ni aina ya gari alilochagua. Maana lilikuwa la kawaida mno, lisilokidhi viwango vya hali ya juu".

Funzo; 
Moja; Kwenye maisha, hakuna juhudi zinaenda bure. Bila kujali muda utakaochukua, lakini matokeo mazuri utayapata.

Mbili; Matokeo ni bora kuliko maneno. Hii ni kwa sababu yanajionesha yenyewe bila wewe kutumia nguvu kujitangaza.

Tatu; Ubora ni sifa inayokuuza mbele ya wengine, bila kujikomba komba mbele ya wengine na utawashida washindani wako.

Kama unataka kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea, katika biashara yako usichoke kutoa huduma bora kwa wateja. 

Usiseme huyu mteja ametuzoea hana shida hata tusipomsikiliza atarudi tena, unajikuta unampoteza. 
Hivyo, kila fursa unayoipata kufanya kitu chochote bila kujali ni wapi na wakati gani, jitahidi kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana. 
Hitimisho; Kama hawawezi kukusifia kwa kazi nzuri unayofanya, jisifu mwenyewe. Kisha, endelea kufanya kazi yako na usubiri muda uongee zaidi na zaidi.

Wako Wa Daima 

Lackius Robert 

Monday, March 20, 2023

Ukifanya hiki utajitoa kwenye mazoea

Imekuwa kasumba kwa wengi wetu hasa mahali pa kazi kukwepa baadhi ya majukumu. 

Wakati mwingine unaenda katika ofisi fulani, ukitaka kupewa huduma fulani. Mhusika unayekutana naye, anakwambia nenda meza ile huyo atamaliza shida yako. 

 Unapochukua hatua ya kwenda kwa huyo mtu uliyeelekezwa labda ni IT au customer care badala amalizie shida yako anakwambia subiri kesho au kesho kutwa kuna mfumo haupo sawa. 

Pengine hamna shida yoyote, amejisikia uvivu tu. Hii hali imekuwa inarudisha nyuma maendeleo yetu kwa kiasi kikubwa. 

Unaenda kwa fundi anakwambia njoo baada ya siku mbili. Ukienda anakwambia umeme ulikata njoo keshokutwa. Ukija anakwambia kuna kifaa kakiagiza mahali. Huo wote ni uvivu tu wa kufanya kitu chako. 

Hii hali inapoendelea kuna watu wanaanza kujitoa taratibu taratibu kwenye biashara au huduma yako. Kwa sababu hakuna kitu wateja au watu wanakwepa kama kuzungushwa mara mbili au tatu. Ukimfanyia hivyo jua umempoteza. 

Ili tuwafanye wathamini huduma zetu, tuache uvivu kama kazi imekuja kwako ifanye kwa moyo wote. Muheshimu aliyeacha kazi zake akaja kwako umfanyie kazi. 

Kama ingekuwa halipi pesa yake sawa. Lakini wanalipa pesa ndicho kinachoumiza moyo. Pesa inatafutwa kwa shida. Hivyo, ukiiheshimu na ukaipokea kihalali watakuheshimu na kukupa kazi nyingi. 

Lijue hili likusaidie kukuza brand yako. Acha uvivu fanya kile kinachowezekana. 

Una changamoto yoyote bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert
Hamasika 2023

Saturday, March 18, 2023

Usichoke, ndiyo maisha yetu


Kauli isemayo ukifaulu mtihani mmoja kwenye maisha usiwadharau waliofeli ni kweli kabisa. Kwa sababu maisha yanayo mitihani mingi sana. 

Unamaliza mmoja, unakuja mwingine zaidi yake. Unakumbuka siku umebanwa na kodi ya nyumba. Ukaumiza kichwa sana kuitafuta ili uendelee kulala chumbani kwako kwa raha mstarehe. Ile umemaliza kuilipa hivi, ukaambiwa mama anaumwa inatakiwa pesa ya matibabu. 

Ile furaha na amani uliyokuwa unaitegemea ilipotea ghafla. Pengine ukajisemea hii pesa inanipa furaha bandia. Nimekamilisha moja limekuja jingine. 

Umemaliza elimu ya chuo kikuu, ukiwa na dhana ya kwamba maisha umeyaweza. Hakuna kingine cha kukupa shida. Mara unakutana na janga la ukosefu wa ajira. Huu ni mtihani mwingine mkubwa. Unaanza kupigana nao. 

Umefanikiwa kuingia kwenye ndoa ukasema sasa mateso basi. Amani, furaha na starehe vinaanza. Majukumu yanapoanza kuwa mengi unajiuliza wapi pa kupumulia. Mke anataka hitaji hili, mtoto anataka hitaji lingine. Ndiyo maisha yetu. 

Pengine, umefanikiwa kununua gari ukasema; kuninginingia kwenye daladala basi. Ulipoipeleka garage gharama za vifaa na mafuta jasho linaanza kukutoka. Mawazo mengi juu ya services zake. Ndiyo maisha yetu ndugu. 

Sasa unafanya nini katika hali hiyo. Ni kitu kimoja unachohitaji na kitu hicho ni maandalizi. 

Uzuri wa kuwa na maandalizi katika kila kitu unachofanya yanakusaidia kupunguzwa uwezekano wa kushindwa. Ndio maana upo msemo wa wakati wa vita sio wakati wa kujiandaa. Bali kabla ya vita ndiyo wakati sahihi wa kujiandaa. 

Hata kwenye maisha yetu ndivyo ilivyo. Unahitaji kuwa na maandalizi ya kutosha kabla hujaanza kufanya kitu. Maisha yanatufundisha kila siku na mitihani tunayofanya ni majukumuku na kazi zetu za kila siku. 

Usiache kujiandaa na mambo yataenda vema. 

Una changamoto yoyote bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
Hamasika2023

Friday, March 17, 2023

Nini kinafanya wakuchague?


Siku moja nilialikwa na taasisi moja kwa ajili ya kusimamia zoezi la usaili wa kazi. Kwenye jopo tulikuwa watu wanne . Kwa sababu mimi ni mtaalamu katika masuala la Sheria za Kazi na Ajira. Walinipa nafasi kubwa na wote walikuwa wanasikiliza neno la mwisho kutoka kwangu. 

Usaili kiukweli ulienda vizuri, nikiwa makini sana kuhakikisha anapatikana mtu sahihi. 

Wakati tunaendelea na usaili kuna dada mmoja tumuite Mwajuma japo sio jina lake halisi aliingia akaanza kujielezea background ya elimu na ujuzi wake. 

Kikafika kipindi cha maswali nikamuuliza swali la kwanza. Je, unajua nini kinafanya tukuchague wewe? 

Mwajuma akasema, ni Kwa sababu mkinichagua nitaweza kumsaidia baba yangu anayeumwa nyumbani. Matibabu yatatokana na mshahara mtakaonilipa. 

Nilimwambia tumekusikia. Nikashika kichwa na kujiuliza maswali mengi. Je, huyu anajua anachofanya? Na hiki alichosema anakijua au amesahahu kwamba  hakuna mtu anayekupa kazi kama msaada. 

Baadaye wakata tutoe hitimisho juu ya usaili mzima. Binafsi nilimwambia bosi kwamba mtu pekee mwenye sifa alikuwa ni mmoja tu Mwajuma. Ila tatizo ni moja. Ajajua ni kwa nini anatafuta kazi. 

Kwa hiyo either mtangaze upya au mchukue Mwajuma kisha muelekeze namna bora ya kufanya kazi. Mwambie hupewi kazi kwa sababu ya matatizo uliyo nayo au kama msaada bali ujuzi na namna unavyoweza kuisaidia taasisi kuzalisha zaidi. 

Note: Ukiwa unaomba kazi mahali popote pale, elezea namna utakavyofanya kazi hiyo kwa ufanisi, uadilifu na faida utakayoongeza. Na sio unavyotaka kutatua matatizo yako kupitia kazi.

Usiseme  nina mtoto mdogo na hakuna wa kunisaidia. Ninataka kujikimu kimaisha. Baba yangu anaumwa au mama yangu au kwa sababu nipo tu nyumbani.

Waambie ninaweza kufanya 1, 2, 3 na nipo tayari kufanya kazi kwa jitihada zote ili kuhakikisha kampuni au biashara hii inafikia hatua nzuri.

Sehemu nyingi za kazi wanatafuta wafanyakazi wanaoenda kuleta suluhu na sio kuongeza matatizo. Ikiwa umepata nafasi, usiichezee tena umefika kwenye usaili wa kuongea. Hupaswi kutia doa. 

Funguka onyesha ujuzi wako, hadi wanaofanya usaili washangae. Hii itafanya waone kitu cha ziada kwako. 

Waonyeshe namna unavyoenda kukuza uzalishaji katika kampuni au taasisi husika. Itakutofautisha na wengine. 

Umewahi kukataliwa mahali kisa huna vigezo, ulijua kwa nini? 
Bonga nasi hapa hapa 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
Hamasikaacademy2023

Thursday, March 16, 2023

Nguvu ya jina la kwanza

Helow! Robert, habari yako? 
Helow Lackius, habari yako? 

Hawa ni watu wawili tofauti wanaopiga simu kwa wakati tofauti. Ila attention inachukuliwa na kwa mtu wa pili. Unataka kujua kwa nini? 

Kuna nguvu kubwa ya kutaja jina la kwanza la mtu. Inaonyesha kabisa unamfahamu. Hata kama umepewa namba na mtu ila akakupatia majina mawili, ukitaja jina lake la kwanza. Kuna umakini mkubwa unautengeneza kwake. Mtu aliyepigiwa anaitwa Lackius Robert. 

Ipo hivi sauti ambayo mtu anapenda kuisikia mara nyingi ni jina lake. Hata kama yupo sehemu yenye kelele kubwa, ila akisikia jina lake lazima aweke umakini mkubwa. Hii ni kwa sababu ndiyo sauti anayopenda kusikia. 

Unapokuwa umetaja jina la pili, anakuwa na wasiwasi ikiwa unamjua vema. Anaweza kuhisi kuna umakini fulani unaukosa. Sio kwamba hawezi kuendelea kukusikiliza ila unapokuwa umetaja jina la kwanza anaongeza umakini mkubwa. 

Ukitaka kujua hili, piga simu kwa mtu uliyepewa namba yake akiwa mpya. Anza kutaja jina lake la kwanza utaona namna atakavyoruhusu mazungumzo yenu. 

Wewe timiza hili, taja jina lake la kwanza mara zote unapoongea na mtu. Iwe ni mteja, rafiki au mtu mwingine, usiache kumuita jina lake la kwanza. Ndio siri kubwa iliyofichwa kwenye jina la kwanza. 

Kingine cha kuzingatia ni kutaja jina lake kwa ufasaha zaidi. Epuka kukosea jina la mtu wakati wa kulitaja. Mfano anaitwa Lackius. Epuka kutumia Lackilius utaondoa umakini wake ataona ujali na huna umakini hata kidogo. 

Unapata changamoto yoyoye bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
Mwangaza 2023

Monday, March 13, 2023

Unaweza kushinda mchezo wowote

Napoleon Hill kwenye kitabu chake cha "Think and Grow Rich" anasema "washindi kwamwe hawaachi kufanya". 

Hii kauli inatosha kukupa nguvu na imani kuwa unaweza kuwa mshindi katika mchezo wowote. Iwe mpira, biashara, muziki au kitu kingine. 

Ikiwa unacheza mpira, kama utaendelea kufanya mazoezi bila kuacha. Kujifunza mbinu mpya na kuwa na nidhamu bora hakuna namna utashindwa kufunga magoli mengi zaidi. 

Upo kwenye biashara, ushindi wako ni mauzo. Maana kupitia mauzo ndipo pesa hupatikana. Ushindi huo unaenda kuupata pale ambapo utaamua kufanya endelevu bila kuacha. Unajifunza mbinu mpya za masoko kila siku. Hapo lazima uuze na mchezo wa mauzo kwako itakuwa raha maana utakuwa ni mshindi. 

Upo kazini, ikiwa utaonyesha kujali, kujituma, kuwa na nidhamu na kumaliza kazi kwa wakati. Lazima uwe mshindi katika kazi zako. Maana kupitia nidhamu utajiboresha na kukamilisha kazi zako kwa muda muafaka. 

Ushindi ninaozungumza hapa sio tu wa goli kusema wachezaji ndio wanaostahili kushinda la asha! Ni ushindi katika kazi zako. 

Hawajibu message piga simu. Hawajapokea simu watembelee. Mara zote hakikisha kuna kitu kikubwa unakifanya ukilinganisha na hapo awali. 

Mwanamziki piga kazi zaidi. Jifunze na andaa muziki wenye maadili ili watu wote waweze kupata ujumbe. Kuwa mvumilivu usikate tamaa haraka sana. Ushindi kwenye mziki ni wako. Endelea kuonyesha juhudi kubwa. 

Changamoto ni nyingi tunapitia, wewe fanya tu, timiza wajibu wako kufanya. Kama ni simu 20 wewe piga, kama ni kuwatembelea watu 10 kwa siku ili uwauzie wewe nenda. Kama ni mazoezi wewe nenda. 

Hakikisha mara zote, unakuwa kazini. Fanya bila kuchoka. Unaambiwa mchumia juani ulia kivulini. Wakati ndio huu ushindi wako unakaribia. Kila lakheri.

Je, ni nini kinakukwamisha  ushindi wako kwenye kazi zako? 

Bonga nasi hapa hapa 0767702659 

Imeandaliwa na Lackius Robert 
Karibu sana tujifunze zaidi. 

Saturday, March 11, 2023

Mabadiliko yanaanza na wewe


Kama kitu kimetengenezwa kinaweza kubadilishwa. Kama kitu kina uhai kinaweza kubadilika kwa hali fulani fulani. 

Chukulia mtoto mdogo anapozaliwa, haanzi kuongea, kutembea au kuwa na meno. Kadiri muda unavyokuwa unasogea ndivyo anavyokuwa anabadilika mdogo mdogo. 

Chukulia mti wa Mbuyu, mwanzoni huwa unaanza kama mchicha. Wakati huo umbo likiwa dogo sana kadiri muda unavyokuwa usogea ndivyo hubadilika pia. Hadi kuwa na umbo kubwa. Ukiambiwa ulikuwa katika umbo dogo unaweza usikubali lakini huo ndio ukweli. 

Ipo hivyo kwenye maisha yako. Hutaweza kubadili mwili au kujiongezea kiungo kingine kwa maana ya mkono wa watatu au mguu wa tatu la asha! Namaanisha unaweza kuibadili hali ya sasa kuwa bora zaidi. 

Huwezi kuibadili jana ila unaweza kuitumia leo kuiboresha kesho yako. Mabadiliko yote haya yanaanza na wewe mwenyewe. Kukubali kuwa kuna mahali unataka kufika. Kuna kitu unataka kukipata katika maisha yako. Kuna hatua kubwa unataka kuipiga. 

Huo ndio ukweli ninaotaka uweze kuujua "any changes starts with you" mabadiliko yoyote yanaanza na wewe. 

Unataka kubadilika kifikra, kimawazo, kimtazamo na kihisia pia. Hii itakusaidia kuwa tayari kutimiza wajibu wako. Kumaliza kile ulichokianza, bila kujali ugumu kiasi gani unapitia. 

Matumaini unayotaka kuwa nayo. Kuwa tayari kupata habari zaidi. Usipoamua kufanya kitu tambua kuwa wewe ndiye muongozaji katika njia yako. Mafanikio unayotaka yanaanzia kwenye akili yako. Unapaswa kuwa tayari kubadilika kimwili na kiroho pia. 

Ni mengi unahitaji kufanya, wakati ndio huu kuyafanya. Hakuna wa kukuzuia kuyafanya. Ni wewe tu kukubali kubadilika na mabadiliko ya kweli unayotakiwa kuyapata yaanzie akilini mwako. Namna unavyoishi kuwa mtu mwenye focus, weka lengo kutimiza malengo. 

Hiyo yote ukiifanikisha amini maisha yako yatabadilika. Usijali kuhusu muda. Wewe jali juhudi unazoweka kuendana na mabadiliko hayo. 

Kumbuka, Umri sio shida. Kipato chako, mahali unapoishi vyote hivyo havina shida. Ukitaka kubadili chochote anza na wewe. Usikimbilie kutoa lawama kwa watu. Huenda walichangia kuanguka kwako lakini hiyo haiwezi kukuzuia kupata unachotaka.Badilisha mawazo na akili yako na kufanya kile kilicho sahihi. Hakika utafanikiwa. 

Je, ni kitu gani kinakuzuia kuendana na mabadiliko? 

Bonga nasi hapa hapa 0767702659 
Imeandaliwa na Lackius Robert