Monday, January 30, 2023

HUWEZI KUFANANA NA SISI

Habari za Leo ndugu yangu mpendwa: Kuwa makini sana na safari yako. Weka akilini kuwa, kila mmoja anayo matamanio yake na kila mmoja anayo njia anayoitumia kufika kule anakohitaji. Wapo anaotumia pesa, akili au nguvu. Ni vema kutambua nyezo utakayotumia kufika huko. Binadamu tumeumbwa na utofauti katika mahitaji na uelewa wetu. Hitaji langu sio sawa na hitaji lako. Fuatilia hadithi hii ya Mbwa Mwitu na Digidigi. Lipo jambo utajifunza: 

" Siku moja Mbwa Mwitu alikuwa katika harakati zake za kutafuta chakula msituni. Alikutana na kundi kubwa la Digidigi. Katika kundi lile, kila mmoja alikuwa anakula majani kwa “style” yake. Mbwa Mwitu alikaa pembeni akiangalia wanavyokula majani huku wakichezacheza kurukaruka. Alitamani sana Maisha yale. 

Kilichomtamanisha ni kuwa; Watoto wa Digidigi walikuwa mbele huku mama zao wakiwa nyuma. Wanacheza na kula mbele ya mama zao, ili ikitokea hatari waweze kunusurika. Mbwa Mwitu alikatisha mawindo yake na kutamani sana kujiunga nao, yaani kuwa kama wao. Hivyo, aliomba nafasi ya kuonana na kiongozi wao. Alipofika na kuongea naye alisema; nimekuwa nikitamani kwa muda mrefu kuungana nanyi. Leo naomba mnikaribishe rasmi niwe nanyi maana nimependa “life style” yenu umoja na mshikamano. 
 
 wa Digidigi akamuuliza Mbwa Mwitu; mbona hufanani na sisi? Mbwa Mwitu akajibu; nitajitahidi kuchonga na kuweka vipembe vidogo vidogo kichwani na kupunguza mkia wangu na masikio yangu. Pia nitajifunza kula nyasi ili niweze kuendana nanyi. Kiongozi wa Mbwa Mwitu akasema; sawa! Nenda ufanye hivyo, kisha urudi nione utakavyokuwa unafanana. 

 Mbwa Mwitu akafanya kama alivyoambiwa, kisha kurudi kwa kiongozi wa Digidigi. Alipofika alisema; Mheshimiwa tayari nimeshajiweka vizuri. Ona nimepunguza mkia wangu, nimechongesha vipembe na kupunguza upana wa masikio yangu. Lakini kiongozi alivyomtazama akamwambia; huwezi kufanana na sisi. Miguu yako haina kwato kama yetu. Mdomo wako upo tofauti na wa kwetu. Isitoshe, ngozi yako ni tofauti na yetu. Sisi hatuna mabakamabaka kama uliyonayo wewe. Sauti yako ni ya kubweka tofauti na ya kwetu. Tafadhali, tunaomba uondoke hapa. 

Mbwa Mwitu aliondoka akiwa amenyong’onyea kurejea kwa Mbwa Mwitu wenzake. Alipofika walimkataa, kwa sababu tayari alishabadili mwonekano wake kuanzia kwenye masikio na mkia walimwambia ondoka kwetu. Wewe sio mwenzetu umetusaliti. Mbwa Mwitu aliondoka akiwa na machungu mengi na kutokomea kusikojulikana."

Tunachojifunza katika hadithi hii ni kuwa; katika safari yetu ya kuelekea tunakohitaji, ambapo ndipo ndoto yetu ilipo, tunapaswa kuthibiti baadhi ya tamaa zinazoweza kutupoteza na kufanya tutoke kabisa katika mstari wetu wa utafutaji. Tunapaswa kutoendekeza kuishi au kufanya kama wengine wanavyofanya, bali tuweke nguvu katika vile tunavyoona ni sahihi kutufikisha tunapokwenda.

Maelezo zaidi nimeweka katika kitabu Cha Ndoto Ya Maisha Yako. 
Karibu sana tujifunze zaidi. 

Mimi ni Lackius Robert
0767702659
#mwangaza2023. 

No comments:

Post a Comment