Tuesday, August 27, 2024

Fanya Kazi Kwa Ubora, Matokeo Yatakulipa Yenyewe

Ndugu, 
Karibu katika mwendelezo wa masomo yetu hapa.

Leo tutajifunza namna gani unaweza kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu ili kujiweka karibu na wateja wako. Tutaanza na simulizi, kisha tutaangalia hatua za kuchukua.

"Ilikuwepo kampuni moja ya uuzaji wa magari, katika kampuni ile, alikuwepo dereva hodari ambaye alisifika kwa kuendesha vema na kuwasimia vema madereva wengine.

Dereva huyo alifanya kazi kwa muda mrefu sana katika kampuni ile. Katika nyakati tofauti tofauti alihitaji kuongezewa mshahara, lakini bosi wake alionekana kama
vile hajali kabisa na hana mpango wa kumwongezea mshahara hadi ulipobakia mwezi mmoja kwa yeye kustaafu.
Kabla ya muda kufika, Mkurugenzi alimwita dereva Juma na
kumwambia kuwa kuna tenda imepatikana ya kuuza gari, naye angependa ampe hiyo tenda
aisimamie iwe ndio kazi yake ya mwisho katika kampuni ambayo pia ingeacha alama yake.

Dereva Juma alikubali kwa shingo upande na akawa analalamika kwa kila mtu pale ofisini kuwa bosi wake hana utu na anaendelea
kumfanyisha kazi bila hata kumwongezea mshahara kama alivyomwomba.
Basi, alienda kuchagua gari zinazoweza kuwa imara kwa ajili ya kuziuza. Kwa kuwa alikuwa ameshavunjika moyo, hakutafuta gari imara, ili amkomoe mkurugenzi washindwe tenda hiyo.
Dereva Juma akawasiliana na 
mkurugenzi kuwa gari la sample limepatikana na atapita juu kwa juu kwenda kwenye sehemu husika waliyotangaza tenda. 
Dereva Juma alipofika sehemu husika, alishangaa kumuona Mkurugenzi na wafanyakazi wenzake na sio wateja kama alivyofikiri.
Dereva Juma akafika, akashangaa watu wanashangilia gafla Mkurugenzi akaja na kumwambia Dereva Juma; Kuanzia sasa hii gari ni yako, ni shukrani yangu kwa muda wote ambao umefanya kazi katika kampuni yetu.
Wakati wafanyakazi wanashangilia yeye alianza kulia. Kilichofanya alie ni aina ya gari alilochagua. Maana lilikuwa la kawaida mno, lisilokidhi viwango vya hali ya juu".

Funzo; 
Moja; Kwenye maisha, hakuna juhudi zinaenda bure. Bila kujali muda utakaochukua, lakini matokeo mazuri utayapata.

Mbili; Matokeo ni bora kuliko maneno. Hii ni kwa sababu yanajionesha yenyewe bila wewe kutumia nguvu kujitangaza.

Tatu; Ubora ni sifa inayokuuza mbele ya wengine, bila kujikomba komba mbele ya wengine na utawashida washindani wako.

Kama unataka kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea, katika biashara yako usichoke kutoa huduma bora kwa wateja. 

Usiseme huyu mteja ametuzoea hana shida hata tusipomsikiliza atarudi tena, unajikuta unampoteza. 
Hivyo, kila fursa unayoipata kufanya kitu chochote bila kujali ni wapi na wakati gani, jitahidi kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana. 
Hitimisho; Kama hawawezi kukusifia kwa kazi nzuri unayofanya, jisifu mwenyewe. Kisha, endelea kufanya kazi yako na usubiri muda uongee zaidi na zaidi.

Wako Wa Daima 

Lackius Robert